Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ameagiza kuchunguzwa kwa sukari kontena 115 ambayo ni zaidi ya tani 3,000 iliyokutwa katika Bandari Kavu ya PMM iliyopo eneo la Vingunguti.
Makonda alitoa agizo hilo alipofanya ziara ya kushtukiza katika bandari hiyo na kubaini uwepo wa sukari hiyo ambayo ni mali ya Mohamed Enterprises, ambayo kwa taarifa zake aliambiwa zilikuwa kontena 165.
Makonda ameziagiza Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) pamoja na Shirika la Viwango (TBS) kuichunguza sukari hiyo kutokana na sababu mbalimbali zilizojitokeza katika uwepo wa sukari hiyo kama sukari kuagizwa kutoka Dubai lakini imetoka Brazil na imepakiwa Dubai na upangwaji wa kontena hizo katika bandari hiyo.
“Nashindwa kuelewa kwa nini sukari iagizwe kutoka Dubai lakini itoke Brazil na kufungashwa Dubai, inaonesha inaweza kuwa imeshawahi kuisha muda wake hivyo nataka ichunguzwe na tunataka tujue kama Mohamed Enterprises anaficha sukari ili ipelekwe kwa wananchi kwa matumizi,” alisema Makonda.
Mbali na kutoa maagizo hayo, Makonda pia amezuia kutumika kwa sukari mifuko 22,000 iliyokutwa katika ghala la Mohamed Enterprises Tanzania Limited (MeTL) lililopo Barabara ya Nyerere na kutaka wapeleke vielelezo kuhusu sukari hiyo kwa mamlaka zinazohusika kama ya matumizi yoyote.
No comments:
Post a Comment