Mapenzi si kamari, ridhia kwa moyo! Ni sentesi ambayo kama mtu akitafakari kwa kina kuna kitu kitaingia kichwani kwake, kuna baadhi ya watu huwa wanabahatisha katika mapenzi, unakuta mtu anakuwa na mpenzi bila kujua kama anapendwa kweli.
Mapenzi ni ridhaa, yanatokea moyoni,
Unajua moyo wako ndiyo wenye uwezo wa kufanya uchaguzi sahihi na si uchaguzi bali uamuzi wa moja kwa moja, maana moyo ndiyo wenye uwezo wa kupenda na kuhifadhi pendo ndani yake, kabla hujaanzisha uhusiano jaribu kuzingatia yafuatayo kwani Mapenzi ya kulazimisha yana madhara kama ambavyo Mtembezi Mahaba inakudadavulia.
MOYO WAKO UMEMPENDA? Suala la mapenzi uhusisha moyo zaidi, moyo wako ndiyo mwamuzi wa mwisho katika hilo, hata siku moja usikubali kulazimisha moyo wako kwa mtu ambaye hujaridhia kuwa naye, hivyo achana na imani kwamba ukimkataa kijana fulani basi bahati inaweza kukupita; nani amekudanganya?
SI KAMARI
Utakuta msichana anaingia katika uhusiano na mwanaume ambaye hana mapenzi naye ya dhati lakini kwa kuwa mwanaume huyo ana mali na uwezo wa fedha, huamua kumkubali kwa misingi ya kuwa na tamaa ya mali zake, hufanya hivyo akijidanganya kuwa atajifunza kupenda akiwa ndani ya uhusiano na mwanaume huyo kwa maneno mengine, anajidanganya kwamba atacheza kamari ya mapenzi.
MADHARA YA KAMARI YA MAPENZI!
Yapo mengi, lakini kubwa ni lile la kutotosheka na mpenzi uliyenaye; anaweza akakupa kila kitu lakini ukakosa penzi la dhati, ambalo ndiyo msingi wa mapenzi.
Mapenzi ya kweli siku zote utajisikia mwepesi na huru kwa mwenzako, madhara makubwa zaidi ni pale utakapojikuta ukiingia katika uhusiano na mwanaume mwingine kwa ajili ya kusaka penzi la dhati! Unajua kitakachotokea?
Kama hutaleta magonjwa ndani basi siku moja utafumaniwa, kuna siku lazima utafukuzwa nyumbani kwa mwanaume huyo na kama ana hasira, anaweza kukufanyia kitu kibaya, hivyo ni vyema kufanya uamuzi wa busara kwa kuwa na mahusiano na yule akupendaye.